Kesha la Asubuhi Alhamisi, 21/11/2019

KESHA LA ASUBUHI

Alhamisi, Novemba, 21, 2019

VIANGALIENI VILIVYO VYA MILELE

📖"Tusiviangalie vinavyoonekana, bali visivyoonekana, kwa maana vinavyoonekana ni vya muda tu; bali visivyoonekana ni vya milele"📖. 2 Wakorintho 4:18.

✍🏻Kama kanisa litavaa vazi la haki ya Kristo, likajitoa katika kukubaliana na ulimwengu, mbele yake kuna alfajiri ya siku angavu yenye utukufu. Ahadi ya Mungu kwa kanisa itasimama milele. ... Ukweli usioonekana kwa wale wanaoudharau na kuukataa, utashinda. Ingawa wakati mwingine huwa unakawizwa, maendeleo yake hayajawahi kuzuiwa. ...
Kwa kuwa una nguvu ya mbinguni, utapenya katika vizuizi vizito vyenye nguvu kabisa na kushinda kila kikwazo.

✍🏻Kitu gani kilimtia nguvu Mwana wa Mungu wakati wa maisha yake ya taabu na kujitoa? Alikuwa anaona mazao ya taabu ya nafsi yake na kuridhika. Akitazama mambo ya milele, aliiona furaha ya wale waliokuwa wemepata msamaha na uzima wa milele kwa ajili ya kudhalilishwa kwake. Sikio lake lilisikia sauti za waliokombolewa. Aliwasikia waliokombolewa wakiimba wimbo wa Musa na Mwana-Kondoo.

✍🏻Tunaweza kuwa na maono ya siku zijazo, baraka za mbinguni. katika biblia kuna maono ya utukufu ujao, mandahari zilizofanywa kwa mkono wa Mungu, nazo ni za thamani kwa kanisa lake. Tunaweza kusimama kwa imani ukingoni mwa ule mji wa milele, na kusikia ukaribisho wa neema kwa wale wanaoshirikiana na Kristo katika maisha haya, wakichukulia kuwa ni heshima kuteseka kwa ajili yake. Maneno haya yatakapotamkwa, "Njooni, mliobarikiwa na Baba yangu," watatupa taji zao miguuni pa Mwokozi wakisema, "Astahili Mwana-Kondoo aliyechinjwa, kuupokea uweza na utajiri na hekima na nguvu na heshima na utukufu na baraka... Heshima na utukufu na uweza una yeye aketiye juu ya kiti cha enzi, na yeye Mwana-Kondoo, hata milele na milele." Mathayo 25:34; Ufunuo 5:12-13.

✍🏻Huko, waliokombolewa watawapokea wale waliowaongoza kwenda kwa Mwokozi, na kwa pamoja wataungana katika kumsifu yeye aliyekufa ili wanadamu wapate uzima unaofanana na ule wa Mungu. Pambano litakuwa limekwisha. Taabu na migogoro vitakuwa vimefikia mwisho. Nyimbo za ushindi zitaijaza mbingu wakati waliokombolewa watakapoimba ule wimbo, Astahili, astahili Mwana-Kondoo aliyechinjwa, naye yu hai tena, mshindi anayefurahia ushindi.

MUNGU AKUBARIKI UNAPOTAFAKARI NENO LAKE...🙏

No comments

Powered by Blogger.