Siku 10 za maombi: Siku ya Saba - Jumanne - (14/01/2020)

Kuomba katika Roho Mtakatifu
Fungu Elekezi: “Kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika Roho, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote.” Waefeso 6:18

Ushuhuda 
“Kristo, Mpatanishi wetu, na Roho Mtakatifu huomba na kusihi daima kwa niaba ya wanadamu, bali Roho hatuombei kama atuombeavyo Kristo anayewasilisha damu yake, iliyomwagwa tangu misingi ya dunia; Roho hutenda kazi katika mioyo yetu, akitoa maombi na hatia ya dhambi, sifa na shukrani. Shukrani zitiririkazo kutoka kwenye vinywa vyetu ni matokeo ya Roho akigusa nyuzi za nafsi katika kumbukumbu takatifu, akiamsha muziki wa moyo” (Ellen White, SDA Bible Commentary, vol 6, aya 1077-78).

Maombi yanaleta changamoto. Hatuwezi kumuona Mungu, na kwa wengi wetu ni mara chache sana, kama imeshatokea, humsikia Mungu. Hatuwezi kumgusa, na nyakati nyingine huonekana kama vigumu kwa majibu kutokea. Pia tuna maswali mengi sana kuhusu namna maombi yanavyotenda kazi, au kwa nini yanaonekana kutotenda kazi.

Ninakumbuka nilivyoomba kama kijana mdogo na kuwa na hali ya kukata tamaa. Mara nyingi nilisinzia (nikiomba huku nimeinamisha kichwa na kufumba macho), na mara kadhaa akili yangu iliwaza orodha ya mambo niliyohitaji kutenda badala ya kuzungumza na Bwana. Nyimbo kama “Saa heri ya Maombi” zilikuwa ni fumbo kwangu. “Ni kwa namna gani mtu anaweza kuomba kwa lisaa lizima? Ni vigumu kwangu kuomba kwa dakika 15 tu.” Hata hivyo, utafiti mmoja huonyesha kwamba muda wa wastani ambao wachungaji hutumia katika maombi ni dakika 7 hadi 10 kila siku! Ninahisi hatia. Kwa mambo yote ambayo mchungaji anapaswa kuyatenda kwa moyo, maombi ndilo jambo la muhimu Zaidi ya yote.

Nilipokuwa nikijifunza kwa undani mada ya Roho Mtakatifu, nilikutana na fungu hili: “Kadhalika Roho naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa” (Warumi 8:26). Sikuelewa kwa ukamilifu fungu hili kwa wakati ule, lakini ilikuwa wazi kwamba Roho Mtakatifu angenisaidia katika maombi. Wazo hilo moja lilianza kubadilisha maisha yangu ya maombi.
Mungu ameahidi kunisaidia kuomba, hivyo nilianza kudai ahadi hiyo kwa moyo wangu wote. Niliposinzia, nilidai ahadi hiyo.

Akili yangu ilipoanza kuwaza mengine, nilidai ahadi hiyo. Baada ya muda thamani cha maombi yangu na muda niliotumia katika maombi viliongezeka. Pia, nilitumia muda mwingi Zaidi katika maombi, changamoto binafsi zilitatulika au ziliondoka, na miujiza ilianza kutendeka. Siwezi kuelezea ni kwa nini, lakini inaonekana kuwa ni kweli: muda unaotumika katika maombi ni muhimu kama thamani ya kile tunachokinena.

Japokuwa nyakati nyingine maombi bado ni changamoto, huwa ninaona kama muda unasonga haraka, na sina matatizo katika usingizi au kuwaza mambo mengine. Ninafahamu Mungu husikia maombi yangu, na ninafahamu kwamba atajibu kwa wakati na njia yake mwenyewe. Hivyo, tukizungumza kibiblia, kuomba katika Roho humaanisha kufanya jitihada za kibinadamu katika kuboresha muda wetu katika maombi huku tukimuamini Roho Mtakatifu kutuvuvia na kututia nguvu.

Baadhi ya mawazo ya kuboresha katika maisha yako ya maombi: 

  1. Omba kupitia maandiko. Soma fungu na muombe Bwana kuhusu jambo ulilolisoma.
  2. Tumia muziki. Kitabu cha nyimbo za Kristo na vitabu vingine vya nyimbo huwa na maombi mengi sana. Tumia maombi hayo kukusaidia kufahamu unachohitaji kunena. Kuimba ni namna nyingine ya kuomba.
  3. Omba katika eneo lenye hewa safi na mbali na masumbufu.
  4. Andika maombi yako. Watu wengi hufurahia kuandika maombi ya kugundua kwamba huwasaidia kuweka sawa mawazo yao na kujieleza kwa ufasaha Zaidi.
  5. Tafuta mwenzi wa maombi unayeweza kuomba naye ana kwa ana au kupitia simu.
  6. Hudhuria mikutano ya maombi (kanisani au nyumbani) au anzisha mkutano wa maombi.
  7. Andaa orodha ya mambo unayohitaji kuzungumza na Mungu.

Mafungu ya Biblia ya Kuombea

  1. Yuda 20 – Tunajenga Imani yetu kwa kuomba katika Roho Mtakatifu.
  2. Waefeso 6:18 – Omba katika Roho ukiwa na maombi ya aina yo yote.
  3. Luka 6:12 – Yesu alikesha katika maombi.
  4. Luka 11:11-13 – Roho Mtakatifu hutujia kama majibu kwa maombi yetu.
  5. 1 Timotheo 2:1 – Maombi ni jambo la muhimu zaidi tunaloweza kutenda.
  6. Luka 22:43 – Msaada wa kimbingu utasaidia kuimarisha maombi yetu, kama ulivyofanya kwa Yesu. 
  7. Mwanzo 32:24 – Yakobo alipambana na Mungu. Nyakati nyingine maombi huonekana kama kazi ngumu.
  8. Luka 18:1 – Tutabarikiwa ikiwa tutadumu katika maombi bila kufa moyo.
  9. Zakaria 12:10 – Roho ya neema na maombi itamwagwa kwetu na kwa familia zetu.

Mapendekezo ya Maombi

  1. Mpendwa Baba, nifanye kuwa mtu wa maombi na nitumie kuwabariki watu katika maisha yangu. Tafadhali nimwagie Roho wako Mtakatifu na nipatie nguvu.
  2. Bwana, tafadhali kemea Shetani na roho zake za uovu zinazotaka kuniweka kifungoni. Nipatie ushindi dhidi ya dhambi zangu kupitia nguvu ya damu yako. 
  3. Tafadhali okoa watoto na wajukuu wetu. Tuma kila malaika mbingu inayoweza kumtoa ili awaongoze katika uzma wa milele. Vunja nguvu za Shetani dhidi yao, wasaidie waweze kuuona wema wako, na wapatia roho ya kuungama.
  4. Wabariki wachungaji wetu, waalimu, wainjilisti, na washiriki duniani kote kwa roho ya maombi. Tunaomba kwamba sauti ya umoja ya watu wako ifike mbinguni katika wimbo mkuu wa sifa na kusihi.
  5. Bwana, tunaomba ulinzi wako wa watoto na vijana walio katika hatari. Tunaomba uwalinde dhidi ya wale wanaotafuta kuwaharibu.
  6. Tunaomba uwainue wamisionari wa mijini ili kupanda makanisa kwa ajili ya makundi 806 ya watu katika nchi 20 za Divisheni ya Inter-Europe.
  7. Tafadhali inua jeshi la watenda kazi ili kusimamisha makanisa kwa ajili ya makundi 948 ya watu katika Divisheni ya Inter-America
  8. Bwana, tafadhali ongoza maamuzi ya kanisa katika Mkutano wa Uchaguzi wa Konferensi Kuu 2020 (Juni 25 – Julai 4). Tunaomba wajumbe, viongozi, na wageni wajazwe na roho ya uamsho na upendo.
  9. Tunainua majina ya watu saba tuliyoyaandika katika karatasi zetu. Wavute watu hao karibu na wewe.
  10. Mahitaji ya kuombea ya kanisa mahalia:

Nyimbo Zinazopendekezwa

  1. Saa Heri ya Sala #137
  2. Saa Heri ya Maombi #135
  3. Mungu Atukuzwe #3

No comments

Powered by Blogger.